UN: Maisha ya wapalestina Gaza ni magumu

Umoja wa mataifa umesema wapalestina wanaoishi katika ukanda wa Gaza hawajaona mabadiliko katika maisha yao tangu Israel itangaze mwezi juni kwamba italegeza vizuizi vya kiuchumi katika eneo hilo.

Mkuu wa ujumbe wa umoja wa mataifa huko Gaza, John Ging, amesema uchumi wa Gaza hauendelei na amewashutumu waisraeli kwa kupuuza shinikizo kutoka jamii ya kimataifa la kutaka vizuizi hivyo viondolewe.

Image caption Umoja wa mataifa umelaani Israel kwa kuendelea kuweka vizuizi vya kiuchumi Gaza

Israel ilikuwa imeahidi kuruhusu bidhaa zaidi kuingizwa Gaza baada ya shambulio la wanajeshi wake dhidi ya meli zilizokuwa zikijaribu kuvunja vizuizi hivyo na kusababisha maafa.

Msemaji wa Israel amesema eneo la mpaka bado limefungwa kwa sababu Gaza iko chini ya uthibiti wa kundi la wapiganaji wa kiislamu la Hamas.