Man United chupuchupu na Aston Villa

Manchester United ikiwa nyuma kwa mabao mawili kwa bila, walichachamaa na kurejesha mabao hayo wakati walipopambana na vijana wa Aston Villa.

James Collins na Gabriel Agbonlahor kila mmoja alikosa mabao kwa mikwaju iliyogongwa mwamba, kabla ya Ashley Young kupachika bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti.

Marc Albrighton aliifungia Villa bao la pili kwa mkwaju wa karibu na kuifanya timu hiyo iongoze katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya England kwa siku ya Jumamosi.

Lakini Manchester United walicharuka baada ya mabao hayo na alikuwa Federico Macheda aliyeanza kujenga matumaini kwa timu yake, baada ya kupachika bao la kwanza kwa mkwaju mkali na Nemanja Vidic akafunga bao la kusawazisha kwa kichwa baada ya kupokea pasi kutoka kwa Nani aliyechonga krosi murua dakika za mwisho.

Kuchachamaa kwa Manchester United kulifanya pambano hilo lichangamke zaidi dakika za mwisho, lakini meneja wa United Sir Alex Ferguson ni lazima ajiulize kwa nini timu yake ilisubiri hadi dakika za mwisho ndio wacheze soka yao ya kiushindani.

Matokeo hayo bado yanaibakiza Manchester United nafasi ya pili na pointi 25, huku Aston Villa wakiwa nafasi ya nane na pointi zao 17.

Katika pambano jingine Manchester City ilishindwa kupata bao katika mchezo wa tatu mfululizo katika uwanja wa nyumbani walipobanwa na Birmingham na kutoka sare ya 0-0.

Sifa nyingi katika mechi hiyo ziwaendee wageni Birmingham kwa nidhamu waliyoonesha na kujituma, lakini namna City wanavyocheza ni suala litakalokuwa juu hivi sasa katika vyombo vingi vya habari.

Kwa matokeo hayo, Manchester City wapo nafasi ya nne na pointi 22, huku Birmingham, bado wametulia katika nafasi ya 17 na ponti zao 13.

Nayo Tottenham walicharuka nyumbani kwao baada ya kuwachambanga Blackburn mabao 4-2.

Tottenham sasa wamepata pointi 19 na kujisogeza nafasi ya 6 ya msimamo wa ligi kuu ya soka ya England.

Timu nyingine iliyovuna mabao ilikuwa Bolton ambao wakicheza ugenini, walifanikiwa kuwalaza Wolves mabao 3-2.

Bolton wamesogea hadi nafasi ya 5 wakiwa na pointi 19 sawa na Tottenham.

Wolves bado wanasugua nafasi ya 19, nafasi moja kutoka mkiani na pointi zao 9.

West Ham walishindwa kuutumia uwanja wa nyumbani angalao kujinasua kutoka mkiani baada ya kulazimishwa sare na Blackpool. Bado West Ham wanaburura mkia na pointi zao 9. Sare hiyo, Blackpool wamebakia nafasi ya 14 na pointi 15.

Wigan wamejisogeza hadi nafasi ya 16 na pointi zao 14 baada ya kuwalaza bao 1-0 West Brom.

Newcastle walikwenda sare ya kutofungana na Fulham. Matokeo hayo yameifanya Newcastle ifikishe pointi 18 wakiwa nafasi ya saba na Fulham pointi 14 wapo nafasi ya 15.