Haye awataka akina Klitsckho

David Haye amesema atafanya "kila awezalo" aweze kupambana na Wladimir au Vitali Klitschko baada ya kumbomoa Audley Harrison siku ya Jumamosi.

Haye, mwenye umri wa miaka 30, alimsimamisha Harrison katika raundi ya tatu na kuweza kutetea taji lake la uzito wa juu la WBA, pambano lililofanyika mjini Manchester, kabla ya kuelekeza mawazo yake kwa akina Klitschko.

Wladimir ni bingwa wa uzito wa juu wa IBF pamoja na WBO, kaka yake Vitali anashikilia mkanda wa WBC.

Haye amesema:"Mimi ni mtu muhimu na hakuna mwengine wa kupambana nao na nitapambana na mmoja wao."

Haye ilikuwa apambane na Wladimir, mwenye umri wa miaka 34, mwaka jana lakini akalazimika kujitoa kwa sababu baada ya kuumia mgongo na mazungumzo ya pambano hilo yamekuwa yakikwama mara kwa mara tangu wakati huo.

Na wakati Muingereza huyo akisita kutoa ahadi ya pambano lake lijalo kama atawavaa akina Klitschko, yeye pamoja na meneja na mwalimu wake Adam Booth, walikuwa na matumaini hivyo ndivyo itakavyokuwa na wakimtamani zaidi Wladimir kuliko kaka yake mwenye umri wa miaka 39.

Haye anaamini anazo zana za kumchakaza Wladimir iwapo mazungumzo ya kufanyika pambano hilo yatazaa matunda.

"Ninajua namna ya kumpiga," alibainisha. "Hajapigana na mtu yeyote mwenye kasi na nguvu, kile ninachoweza kufanya ni kumtandika ngumi za kichwani na ataangamia kama nilivyomfanya Audley.

Pambano litakalofuata la Wladimir ni dhidi ya Dereck Chisora wa London, ambalo litafanyika tarehe 11 mwezi wa Desemba huko Mannheim Ujerumani, pambano ambalo linatarajiwa Wladimir atashinda kwa urahisi.

Wladimir amekwishashinda mapambano 55 kati ya 58 ya ngumi za kulipwa.