Ugiriki ilikuwa taabani

Umoja wa Ulaya, EU, umefichua kwamba matatizo ya kifedha kuhusiana na madeni ya nchi ya Ugiriki yalikuwa makubwa mno, kinyume na ilivyokadiriwa hapo awali.

Hayo yamejitokeza wakati serikali ya Ireland, ambayo imekumbwa na madeni, imekuwa ikishauriwa na mataifa ya Umoja wa Ulaya, ikubali kusaidiwa kifedha, na uwezekano pia wa shirika la kimataifa la fedha, IMF, kuingilia kati.

Mwaka uliopita mwezi Juni, Umoja wa Ulaya pamoja na shirika la kimataifa la fedha IMF, walitoa msaada wa dola bilioni 146 kuisaidia Ugiriki kulipa madeni yake.

Image caption Waziri mkuu wa Ugiriki

Kufuatia kitendo hiki Ugiriki ililazimika kukata matumizi yake na kupandisha ushuru, jambo ambalo lilisababisha wananchi kuandamana nchini humo.

Wakati huo iliibuka kwamba Ugiriki walitumia ulaghai katika uhasibu wake kuficha kiasi cha shida zilizowakumba.

Leo takwimu kutoka kwa wahasibu wa Umoja wa Ulaya zimeonyesha kwamba upungufu wa fedha nchini humo umefikia asilimia 15.4 ya pato la nchi, yaani GDP, ikilinganishwa na asilimia 13.6 mwezi Aprili mwaka uliopita.

Deni lake sasa ni asilimia 127 ikilinganishwa na pato la nchi.

Hii ina maana kuwa serikali ya Ugiriki haitofaulu kusawazisha upungufu wa fedha unaoikumba bajeti ya nchi hii.