Rais mpya wa Guinea kutangazwa hii leo

Raia wa Guinea
Image caption Raia wa Guinea

Shughuli ya kuhesabu kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa Urais nchini Guinea, inakaribia kumalizika huku matokeo ya awali yakibainisha kuwa wagombeaji wawili wa kiti hicho wanakaribiana sana.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, uongozi wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Cellou Dalein Diallo, unaendelea kupungua kwa kiasi kikubwa.

Mpinzani wake Alpha Conde naye anaendelea kujizolea kura zaidi kadri matokeo hayo yanavyoendelea kupokelewa.

Hapo Jumapili chama cha Diallo kilitangaza kujiondoa katika shughuli hiyo ya kuhesabu kura.

Chama hicho kinadai kumekuwepo na dosari nyingi katika shughuli hiyo ya kuhesabu kura kutoka wilaya tatu.

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa baadaye hii leo.