Jitokezeni kwa wingi kupiga kura - Kiir

Kiongozi wa Sudan Kusini Salva Kiir amewataka wananchi wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kupiga kura ya maoni ya kujitawala yenyewe au la itakayofanyika mwezi Januari.

Image caption Salva Kiir akijiandikisha kupiga kura

Bw Kiir alikuwa akizungumza mbele ya umati wa mamia ya watu katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, baada ya uandikishaji kuanza.

Kura ya maoni ni sehemu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 ya kumalizamiaka mingi ya mapigano ya Sudan Kusini na Kaskazini.

Pande hizo mbili zilikubaliana kuainisha mpaka kati ya Kusini na Kaskazini, na pia kuruhusu wafugaji kulisha upande wa Kusini.

Image caption Salva Kiir

Makubaliano hayo pia yanajumuisha kuruhusu raia wote wa Sudan kuwa na haki ya kuishi Kusini au Kaskazini.

Bw Kiir, ambaye ni kiongozi wa zamani wa kundi la waasi, na ambaye anaongoza serikali ya sasa ya Sudan Kusini, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kujiandikisha.

"Kura ya maoni hutokea mara moja tu. Watu lazima wajitokeze kwa wingi, vinginevyo itamaanisha watu walipigana na kufa bila sababu," amesema Bw Kiir.

wanaharakati wakiwa na vipaza sauti wamepita katika mitaa ya Juba, wakiwataka wakazi kujiandikisha kupiga kura.

Wachambuzi wa mambo wanatarajia kuwa wananchi wa Kusini watapiga kura upande huo kujitenga na kusababisha taifa hilo kubwa la Afrika kuganwanyika mara mbili.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii