Huddlestone kufanyiwa upasuaji

Mchezaji wa kiungo wa Tottenham Hotspur Tom Huddlestone atafanyiwa upasuaji wa kisigino cha mguu, hali itakayomfanya asicheze soka kwa muda wa miezi mitatu.

Image caption Tom Huddlestone

Kiungo huyo atakosa michezo muhimu ya kuwania ubingwa wa Ulaya na halikadhalika Ligi Kuu ya soka ya England, ambapo wakati wa kipindi cha sikukuu ya Krismasi kunakuwa na mechi nyingi.

Uamuzi wa kumfanyia upasuaji umekuja baada ya kufanyika ushauri mkubwa.

"Kufuatia ushauri na wataalam mbalimbali binafsi wa kutibu matatizo ya visigino, imeamuliwa Tom Huddlestone afanyiwe upasuaji," taarifa ya klabu imesema.

Mchezaji huyo ambaye pia huchezea timu ya taifa ya England, amekuwa nguzo kubwa kwa timu yake ya Tottenham msimu huu, ambapo amecheza mechi 16.

Lakini katika wiki za hivi karibuni, alikuwa hachezi muda wote wa dakika tisini, kwa sababu ya tatizo la kisigino, hali iliyomfanya achomwe sindano mara kwa mara.

Kiungo huyo wa zamani wa Derby anaingia katika orodha ya majeruhi wa White Hart Lane, hali inayomfanya meneja Harry Redknapp kuwakosa pia Ledley King, Michael Dawson, Jermain Defoe, Jonathan Woodgate, Aaron Lennon, Jamie O'Hara na Robbie Keane.

Kumkosa Huddlestone kumekuja huku Jumamosi kukisubiriwa pambano la watani wa jadi wa kaskazini mwa London, ambapo Arsenal itawakaribisha Tottenham na pia atakosa mpambano dhidi ya Chelsea, Liverpool na Manchester United.

Zaidi ya hapo atakosa mechi muhimu za Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Werder Bremen na FC Twente katika wiki chache zijazo.