John Terry kutocheza kwa miezi kadha

Nahodha wa Chelsea John Terry huenda akawa nje ya uwanja kwa miezi kadha, akisumbuliwa na matatizo ya neva katika mguu wake wa kuume.

Image caption John Terry

Matatizo hayo ya mguu yalimfanya Terry kutocheza pambano dhidi ya Sunderland siku ya Jumapili, ambapo Chelsea walifungwa nyumbani kwao mabao 3-0 pia amejiondoa katika kikosi cha timu ya taifa ya England kitakachocheza mchezo wa kirafiki na Ufaransa siku ya Jumatano.

Taarifa za Chelsea zimesema: "Huenda akawa nje kwa miezi kadha ingawa haijulikani wazi itachukua muda gani.

"Hatufahamu mzizi wa maumivu yake na kilichobaki kwa sasa ni kuangalia chanzo cha tatizo lake."

Taarifa hizo ni pigo kwa meneja wa Chelsea Carlo Ancelotti ambaye kiungo wake mahiri Frank Lampard naye ni majeruhi, huku mshambuliaji Didier Drogba anacheza licha ya hivi karibuni kukabiliwa na maradhi ya malaria.

Terry, mwenye umri wa miaka 29, tayari amekwishaonana na wataalam mbalimbali wa tiba katika jitahada zake za kupata matibabu muafaka, lakini hadi sasa hakuna mtaalam aliyeweza kugundua tatizo linalomtanza.

Maumivu yamekuwa yakimtatiza mlinzi huyo tangu ulipomalizika msimu uliopita na licha ya kupumzika kwa wiki tatu baada ya kumalizika fainali za Kombe la Dunia na kabla ya kuanza msimu wa ligi wa mwaka huu, tatizo lake halijatambulikana.

Terry aliliambia gazeti la Daily Mail: "Tatizo lilikuwa afadhali hadi wiki mbili zilizopita, lakini tulipocheza na Fulham nilipokuwa katika harakati za kuwania mpira dhidi ya Clint Dempsey ndipo tatizo likarudi upya na sasa limekuwa baya zaidi.