Watu 4 wauawa kwenye ghasia-Guinea

Wanajeshi wakikabiliana na wafuasi wa upinzani
Image caption Wanajeshi wakikabiliana na wafuasi wa upinzani

Watu 4 wameuawa kwenye mapigano makali kati ya wafuasi wa mgombeaji wa kiti cha urais, aliyeshindwa Cellou Dalein Diallo na wanajeshi wa serikali nchini Guinea.

Mshindi wa uchaguzi huo wa urais, Alpha Conde, amesema anataka kuongoza shughuli ya maridhiano ya kitaifa.

Lakini katika mkutano na kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo Generali, Secouba Konate, Bwana Diallo amewashutumu wanajeshi kwa kutumia nguvu zaidi kupita kiasi.

Diallo amesema wanajeshi hao walitumia nguvu kuwatawanya wafuasi wake ambao walikuwa wakiandamana kwa amani.

Utawala wa kijeshi nchini humo umetangaza amri ya kutotoka nje usiku kucha katika maeneo yaliyoathirika na ghasia hizo.

Wakati huo huo Diallo ametoa wito kwa wafuasi wake, kudumisha amani huku akiapa kuwasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo hayo ya urais.