Ghailani apatikana na hatia

Ahmed Khalfan Ghailani
Image caption Ahmed Khalfan Ghailani

Mshukiwa wa kwanza kutoka gereza la Guantanamo Bay kushtakiwa katika mahakama ya kiraia nchini Marekani, amepatikana na hatia ya kula njama ya kushambulia kwa bomu mali ya taifa la Marekani.

Ahmed Khalfan Ghailani, raia wa Tanzania, alishtakiwa kwa kosa la kuhusika katika mashambulizi ya kundi la kigaidi la Al Qaeda, dhidi ya ubalozi wa Marekani nchini Kenya na Tanzania mwaka 1998.

Viongozi wa mashtaka wamesema Ahmed Ghailani, alichangia pakubwa katika maandalizi na mipango ya kundi la Al Qaeda ya kulipua balozi za marekani nchini Kenya na Tanzania.

Watu 224 waliuawa kufuatia mashambulio hayo mawili.

Mahakama hiyo ilifahamishwa kuwa Ghailani alinunua mitungi ya gesi zilizolipuka pamoja la lori iliyobeba vilipuzi hivyo.

Ghailani alikuwa anakabiliwa na mashataka 281 zikiwemo mauaji na jaribio la kuua.

Hatahivyo, Mahakama hiyo ilimpata bw Ghailani na hatia moja pekee ya kupanga kuharibu mali na majengo ya serikali.

Ushahidi uliokuwa umewasilishwa mbele ya mahakama hiyo ya Marekani dhidi ya mshukiwa huyo zimekataliwa na mahakama kwa sababu zilikusanywa na maafisa wa ujasusi wa Marekani CIA, katika magereza yasiyo rasmi nje ya Marekani kwa njia isiyofaa.

Maafisa hao wa ujasusi wanadaiwa kutumia mbinu kali kumhoji mshukiwa huyo,ikiwemo kumtesa ili akiri mashtaka dhidi yake na pia atoe habari zaidi.

Uamuzi huo wa mahakama unaonekana kuwa pigo kubwa kwa utawala wa Rais Barack Obama, wa Marekani na ahadi yake ya kuwafungulia mashtaka washukiwa wote wa ugaidi wanaozuiliwa katika jela la Guantanamo Bay, katika mahakama ya kiraia.

Maafisa wa serikali ya Marekani sasa wanachunguza upya jinsi ya kuendeleza kesi za washukiwa hao wa kigaidi, na hivyo kumaanisha jela hilo la Guantanamo Bay, iliyoko Cuba huenda isifungwe hivi karibuni.