Arsenal, Chelsea zaboronga

Arsenal na Chelsea zimepoteza mechi zake za Jumamosi, baada ya Arsenal kuchapwa mabao 3-2 na Tottenham, huku Chelsea ikichapwa 1-0 na Birmingham City.

Tottenham wakicheza soka murua kipindi cha pili, walifanikiwa kujipanga upya na kurejesha mabao na kujipatia moja la ushindi, ukiwa ushindi wao dhidi ya Arsenal nyumbani kwao katika mechi ya ligi tangu mwaka 1993.

Gunners walianza kupata bao mapema tu dakika ya tisa kipindi cha kwanza baada ya Samir Nasri kumalizia vizuri katika eneo lilliloonekana gumu kufunga, lakini akafanikiwa na Marouane Chamakh aliipatia bao la pili Arsenal baada ya pasi ya pembeni ya Andrey Arshavin.

Spurs walikuja juu katika kipindi cha pili, na alikuwa Gareth Bale aliyefunga bao la kwanza dakika za mwanzo za kipindi cha pili na Rafael Van der Vaart akapachika bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti baada ya nahodha wa Arsenal Cesc Fabregas kuunawa mpira baada ya kupigwa free kick.

Younes Kaboul akamalizia kazi kwa kuipatia Spurs bao la ushindi la tatu kwa kichwa baada ya kuchongwa free-kick.

Kwa matokeo hayo Tottenham wamesogea nafasi ya tano wakiwa na pointi 22.

CHELSEA

Chelsea nayo ikicheza ugenini dhidi ya Birmingham City, iling'an'ganiwa kwa bao1-0 kwenye uwanja wa Saint Andrews.Bao hilo pekee la Birmingham limefungwa na Lee Bowyer.

Chelsea wakicheza chini ya kiwango chao hawakuweza kukabiliana vilivyo na mchezo wa kujihami ambao umechezwa na Birmingam City. Licha ya beki wa kati wa Chelsea, Alex, kuahirisha upasuaji wa goti lake, Chelsea walionekana kutocheza mchezo wa kuelewana.

Huu ni mchezo wa tatu mfululizo wa ligi kuu ya England ambapo Chelsea wanafungwa. Walifungwa na Liverpool, Sunderland na sasa Birmingham City.

MATOKEO MENGINE

Image caption Patrice Evra

Katika michezo mingine, Manchester United imeichapa Wigan kwa mabao 2-0. Magoli ya Manchester City yamefungwa na beki Patrice Evra, na Javier Hernandes.

Hugo Rodallega na Antolin Alcaraz wa Wigan walioneshwa kadi nyekundu katika mchezo huo. Goli la Evra ni la kwanza kwake katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu.

Kwingineko, Blackpool imeilaza Wolverhampton kwa mabao 2-1, Bolton ikaiangushia kisago Newcastle United kwa magoli 5-1. Stoke City nayo imepata ushindi ikicheza na West Brom.

Liverpool nayo ikicheza nyumbani iliizaba West Ham United kwa magoli 3-0. Magoli hayo yamefungwa na Glen Johnson, Dirk Kuyt kwa penati, na Maxi Rodrigues.