Nigeria yakamata dawa za kulevya

Maafisa wa Nigeria wanasema wamekamata dawa za kulevya aina ya herion zenye thamani ya dola milioni kumi za kimarekani.

Image caption Heroine ikiwa shambani

Dawa hizo zilikuwa zimefichwa katika injini za magari, zikitokea Iran.

Idara ya kupambana na dawa za kulevya nchini Nigeria NDLEA imesema maafisa wake wamekamata dawa hizo katika bandari ya Apapa iliyopo mjini Lagos.

Kukamatwa huko kunakuja siku chache baada ya Nigeria kuishitaki Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuhusiana na shehena ya silaha kutoka Iran iliyokamatwa nchini Nigeria.

Bandari za Afrika Magharibi ni kitovu cha kusafirisha dawa za kulevya kuelekea katika soko la nchi za Magharibi.

Msemaji wa NDLEA Mitchell Ofoyeju amesema idara yake ilipata "taarifa nyeti" kutoka kwa "washirika wa kimataifa" miezi minne iliyopita, na ilikuwa ikifuatilia kwa karibu mzigo huo kabla haujawasili.

"NDLEA iliamua kutumia mashine ya kukata vyuma na kukata injini hizo, na kukuta kilo 130 za heroin zimefichwa ndani yake," amesema Bw Ofoyeju.

Image caption Heroin

Msemaji mmoja wa idara ya forodha ya Nigeria ameliambia shirika la habari la AFP kuwa dawa hizo ziliingizwa Nigeria na meli ya kigeni iitwayo MV Montenegro.

Raia watatu wa Nigeria wamekamatwa kuhusiana na dawa hizo.

Mwezi Oktoba, maafisa usalama wa Nigeria walikamata shehena ya silaha katika bandari hiyo.

Mabomu ya roketi, mabomu ya kurusha kwa mkono na milipuko mingine pamoja na silaha mbalimbali, zilikutwa katika kontena lililokuwa limeandikwa kuwa lina vifaa vya ujenzi, likitokea Iran.

Iran imesema kukamatwa kwa silaha hizo ni suala la "kutofahamiana tu" na tayari limekwisha tatuliwa.