Duru ya pili ya uchaguzi Ivory Coast

Kampeni za duru ya pili ya uchaguzi mkuu nchini Ivory Coast zimeanza rasmi huku Rais Laurent Gbagbo akikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mpinzani wake wa jadi Alassane Ouattara.

Image caption Wapiga kura Ivory Coast duru ya kwanza

Shughuli ya upigaji kura itafanyika Jumapili ijayo na inanuia kuiweka pamoja nchi hiyo kwa mara ya kwanza, tangu kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoigawanja na kuacha nusu yake chini ya utawala wa waasi.

Hakuna mgombea wa kiti hicho aliyeshinda kwa kura nyingi katika duru ya kwanza iliyomuacha Rais Gbagbo akiongoza kwa kura chache tu na kufuatiwa na Bw Outtara.

Maelfu ya wanajeshi watapelekwa katika vituo mbali mbali wiki ijayo kwa sababu ni tofauti za siasa za wagombea hao wawili zilizoitumbukiza nchi hiyo katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Takriban watu watano wamejeruhiwa kwenye mapigano kati ya makundi ya vijana wanaowaunga mkono wagombea hao na polisi wakafyatua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya.