Kolo Toure: Wasiojituma wakatwe mshahara

Mlinzi wa Manchester City Kolo Toure amesema klabu hiyo haina budi kuwakata mishahara wachezaji wenzake kama hawachezi kwa bidii.

Image caption Kolo Toure akipewa mawaidha na mwalimu wake

Bilionea Sheikh Mansour anayeimiliki timu hiyo, ameigeuza kuwa ni moja ya vilabu tajiri duniani na ametumia zaidi ya paundi milioni 120 kununua wachezaji wapya msimu huu.

Na mdogo wake Kolo Toure, Yaya inaarifiwa ndiye anayelipwa mshahara mkubwa wa paundi 200,000 kwa wiki.

"Kuna baadhi ya wachezaji hapa, na siogopi kusema, ambao hawajitumi vya kutosha kwa ajili ya timu," alisema Toure.

Manchester City inayocheza Jumapili hii na Fulham ipo nafasi ya tano ya msimamo wa ligi kuu ya soka ya England, lakini tayari imeonekana si timu yenye ukakamavu wa kutosha kuweza kushinda ligi msimu huu.

City ina idadi sawa ya pointi baada ya kucheza mechi 13, kama walizowahi kuwa nazo chini ya meneja wa zamani Mark Hughes msimu uliopita, lakini wameweza kufunga mabao tisa yakiwa ni machache.

Na Toure mwenye umri wa miaka 29, akiwa amechukuliwa kwa kitita kikubwa kutoka Arsenal mwaka 2009, anaamini wachezaji wenzake wanatakiwa kuanza kuthibitisha uwezo wao na pesa nyingi wanazolipwa.

Ameliambia gazeti la News of the World: "Wapo wachezaji ambao hawaoneshi bidii mazoezini, lakini wanatarajia kucheza. Sote tunapokea mishahara mikubwa, lakini baadhi yetu wanahitajika kufanya bidii zaidi.