Rudisha na Vlasic wanariadha bora

Bingwa mbio za mita 800 duniani kutoka Kenya David Rudisha na bingwa wa dunia wa kuruka juu kwa michezo ya ndani, Blanka Vlasic wa Croatia wametajwa wanariadha bora wa mwaka wa Chama cha Riadha cha Kimataifa Duniani-IAAF.

Image caption David Rudisha

Rudisha, mwenye umri wa miaka 21, mara mbili mwaka huu alivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 800, akiishusha kwa dakika moja sekunde 41.01, ukiwa ni ushindi wake wa mara ya 11 kwa msimu huu.

Vlasic, mwenye umri wa miaka 27, alishinda mashindano 18 kati ya 20 na akaeleza ulikuwa ni msimu mgumu kwake.

Mkimbiaji wa Marekani wa mbio fupi Tyson Gay, Mmarekani mwengine wa mbio fupi kuruka viunzi David Oliver, mkimbiaji wa mbio ndefu kutoka Eritrea Zersenay Tadese na mrusha mkuki Andreas Thorkildsen wa Norway walikuwa miongoni mwa wanariadha wanaume waliofika hatua ya fainali ya mchujo katika sherehe za tuzo hiyo ya wanariadha wa dunia iliyofanyika Monaco.

Vlasic amempiku mwanariadha wa Marekani Sanya Richards kuwa mwanariadha bora kwa upande wa wanawake duniani. Wengine waliofika hatua ya mchujo wa fainali kwa wanawake walikuwa mwanadada wa Jamaica wa mbio fupi Veronica Campbell-Brown, Mmarekani wa mbio fupi Allyson Felix, bingwa wa michezo mitano ama heptathlete wa Uingereza Jessica Ennis na Mkenya wa mbio ndefu za kuruka viunzi na maji Milcah Chemos Cheywa.