Watu wengi watahamia mijini

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imetabiri kuwa idadi ya watu wanaoishi katika miji ya Afrika itaongezeka mara tatu ya idadi iliyopo katika kipindi cha miaka 40 na ifikapo mwaka 2050 asili mia 60 ya raia wa Afrika watakuwa wakaazi wa mijini.

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo mji wa Lagos utauzidi mji mkuu wa Misri, Cairo kuwa mji mkubwa zaidi ya yote barani Afrika.

Image caption Mji wa Lagos kuzidi yote

Kutokana na takwimu hiyo Mkuu wa idara ya makaazi ya Umoja wa Mataifa Joan Clos amesema kuwa itabidi Afrika iwekeze zaidi katika ujenzi.

Bw.Clos ameiambia BBC kuwa sehemu za Afrika zilizoko kusini mwa Jangwa Sahara zinaweza kujifunza kutoka Mataifa ya kaskazini kama Misri, Libya, Morocco na Tunisia ambazo zimepunguza maeneo ya madongoporomoka katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Takriban watu milioni 19.5 walioko kusini mwa jangwa Sahara wanaishi katika mazingira mabobu na idadi yao ni kubwa kuliko sehemu nyingine duniani.

Mafuriko pwani

Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2010 ya shirika la makaazi la Umoja wa Mataifa uhamiaji wa mijini barani Afrika, inafanyika kwa kasi ya kupindukia.

Hadi mwaka 2030 watu wengi watakuwa wakiishi mijini na siyo vijijini.

Image caption Mji wa Kinshasa kutoka mto Congo

Bw Clos, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la makaazi la Umoja wa Mataifa, amesema kuwa miji imekuwa kivutio kwa wanaotaka kuhama. ''Watu wanatafuta maisha bora na wanahisi kuwa hali yao kuwa bora lazima wahamie mijini''

Mageuzi katika Kilimo na umasikini ni sababu nyengine zilizosababisha mtiririko huo, alisema.

Huduma muhimu

Miji mingi hata hivyo inakabiliwa na matatizo ya kurundikana kwa watu, ukosefu wa maji,umeme na mifumo mibovu ya usafiri.

Mbali na hayo maisha ya mijini kawaida hutoa fursa ya maisha bora,ikiwa hatua zinachukuliwa kutoa huduma muhimu kama nyumba na afya, alisema Bw.Clos.

Ifikapo mwaka 2015 inakadiriwa kuwa mji wa Lagos utakuwa na wakaazi milioni 12.4.

Image caption Miji ni kivutio kwa maisha bora

Umoja huo pia unatabiri kuwa idadi ya watu katika mji mkuu wa Jamhuri ya Congo,Kinshasa utaona ongezeko la asili mia 46 katika kipindi cha miaka 10 ijayo na kuwa mji unaokuwa kwa kasi zaidi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo hadi mwaka 2050, idadi ya watu barani Afrika inatazamiwa kufikia watu bilioni 1.23.

Taarifa hiyo inaonya kuwa uharibifu wa mazingira nao umezua matatizo makubwa kwa baadhi ya miji.

Huku miji mingi ya Afrika ikiwa imejengwa pwani, kuna hofu ya mamilioni ya watu kupoteza nyumba zao katika miongo ijayo kutokana na mafuriko.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo pwani ya Afrika ya magharibi inazidi kumomonyoka kwa mita 20 hadi 30 kila mwaka.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii