IOC yachunguza madai ya rushwa Fifa

Kamati ya Kimataifa ya Olympic- IOC itachunguza madai ya BBC dhidi ya Makamu wa Rais wa Fifa Issa Hayatou, ambaye pia ni mjumbe wa IOC.

Image caption Maafisa wa Fifa wanaotuhumiwa kwa rushwa

Kamati hiyo imeiomba BBC kuipatia ushahidi wa tuhuma za rushwa walizopokea maafisa watatu waandamizi wa Fifa, kufuatia madai ya kipindi chake cha Panorama.

Panorama ilidai Bwa Hayatou na maafisa wengine wawili wa Fifa walipokea rushwa kwa ajili ya kupiga kura kwa ajili ya Kombe la Dunia katika miaka ya 1990.

Fifa, ambalo ni Shirikisho linalosimamia mchezo wa soka duniani, limekanusha tuhuma hizo.

IOC imesema itawasilisha suala hilo mbele ya kamati yake ya maadili.

Fifa imetoa taarifa inayosema, tuhuma hizo zimeelekezwa kwa matukio yaliyotokea kabla mwaka 2000 na yamechunguzwa na serikali ya Uswiss.

"Katika hukumu yake iliyotolewa tarehe 26 mwezi wa Juni, 2008, Mahakama ya uhalifu ya Zug haikumtia hatiani afisa yeyote wa Fifa. Kwa hiyo ni muhimu kusisitiza kwa mara nyingine ukweli uliopo hakuna afisa yeyote wa Fifa aliyetuhumiwa na kosa lolote la uhalifu aliyepatikana na hatia." Taarifa hiyo ya Fifa ilieleza.

Kipindi hicho cha Panorama cha BBC, kilichotangazwa siku ya Jumatatu, kilitoa tuhuma kwamba maafisa wa Fifa Issa Hayatou - ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika, Caf raia wa Cameroon - Nicolas Leoz, kutoka Paraguay, na Ricardo Teixeira, kutoka Brazil, walipokea rushwa kutoka kampuni moja ya kibiashara ambayo ilipatiwa mkataba mnono wa haki za kuonesha Kombe la Dunia.

Maafisa hao watapiga kura wiki hii kuamua nchi gani zitandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022.

Hata hivyo maafisa hao wa Fifa hawajajibu chochote kuhusiana na madai hayo ya Panorama.