Waziri Mkuu wa Kenya alaani mashoga

Raila Odinga
Image caption Wanaharakati wa kutetea wapenzi wa jinsia moja wanasema kauli hiyo huenda ikachochea mashambulizi dhidi yao

Waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga amesema nchi hiyo haipo tayari kuwatambua wapenzi wa jinsia moja.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika eneo la bunge mjini Nairobi, Bw Odinga alisema suala la wapenzi wa jinsia moja lilitumiwa kama propaganda kupinga katiba mpya.

Waziri Mkuu huyo amesisitiza katiba mpya ya Kenya haikubali kuwepo wapenzi wa jinsia moja. Na amependekeza wapenzi hao wa jinsia moja wakamatwe na polisi endapo watajitokeza hadharani.

Lakini kauli hiyo imepingwa na David Kuria, mwanaharakati wa kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja.

Bw Kuria ameiambia BBC kuwa kauli hiyo itaathiri kampeni zao za kutetea haki sawa za huduma ya afya kwa watu hao, hasa kuhusu suala la kudhibiti maambukizi ya Ukimwi.