'Afrika yaweza kujilisha'

Afrika ina uwezo wa kujilisha yenyewe na pia ikazalisha chakula cha kutosha kuuza nje.

Hayo ni kwa mujibu wa kitabu kipya kilichozinduliwa hii leo na professa wa chuo kikuu cha Havard Calestous Juma.

Image caption Kilimo

Kitabu hicho, The New Harvest, kinatoa wito kwa viongozi wa Afrika kutilia mkazo upanuzi wa kilimo kupitia sera na mikakati yao ya kitaifa.

Kuafikia hilo, viongozi wa Afrika watahitaji kuboresha miundo mbinu, kutumia teknologia ya kisasa pamoja na kuhimiza kilimo cha mazao ya kufyatua kisayansi, yaani GM.

Ripoti hiyo itawasilishwa kwa viongozi wa Afrika siku ya Ijumaa nchini Tanzania.

Marais wa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi wanafanya kikao kuzungumzia usalama wa chakula pamoja na suala la mabadiliko ya hali ya anga.

Akizungumza na BBC kabla ya mkutano huo, Professa Juma alisema viongozi wa Afrika hawana budi kutambua uhusiano wa kilimo na uchumi wa Afrika.

''Ni jukumu la viongozi wa Afrika kuuboresha uchumi wao na hiyo inamaanisha kuanza kutumia teknonologia ya kisasa katika kilimo'', alisema.

Kwa mujibu wa Professa Juma, uzalishaji wa chakula duniani unaendelea kuongezeka lakini katika maeneo mengi ya Afrika hali ni tete licha ya kuwepo na ardhi ya kutosha ya kilimo.