Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa

Wanyimeni mambo

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, juzi Alhamisi, amewataka wafuasi wake wa kiume kufanya mgomo wa kutoa unyumba kwa wake zao, mpaka pale wake zao hao, waahidi kutokipigia kura chama tawala katika uchaguzi ujao.

Image caption Unataka mstari mwingine??

Wachambuzi wengi wanaamini uchaguzi wa mwezi Februari utamrejesha tena madarakani Rais Yoweri Museveni na chama chake cha National Resistance Movement NRM. " Nyie mnasema ni wafuasi wa upinzani, wakati wake zenu wanakipigia kura chama cha NRM," amesema mwanasiasa huyo Stanley Kalembaye, akizungumza na kundi la watu katika mkutano ambao pia ulirushwa kupitia kituo cha televisheni cha NTV. "Mimi napendekeza muwanyime wake zenu haki ya ndoa ili wabadili vyama." amesema mwanasiasa huyo.

Image caption Jiji la kampala

Shirika la habari la Reuters limesema mgombea huyo wa chama cha MDC ambaye anawania umeya wa jiji la Mbarara, amesema wanaume hawana budi kuwaelewesha wake zao.

"wakishindwa kuelewa kwa njia ya mazungumzo, basi wawanyime unyumba." amesema mgombea huyo.

Migomo ya kunyima unyumba imekuwa silaha inayotumika sehemu kadhaa barani Afrika, lakini mara nyingi huwa ni wanawake dhidi ya wanaume.

Maelfu ya wanawake wa Kenya mwaka jana walidai kuwanyima haki hiyo wanaume zao ili kushinikiza kumalizika kwa ghasia baada ya uchaguzi, huku wanawake wa Liberia pia wakifanya hivyo katika kampeni inayosemwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda mrefu.

Nafikiria -- Kama NRM nao wakiamua kutumia mbinu hiyo, sijui itakuwaje.....

Adhabu ya kupanda behewa la kike

Kundi la wanaume waliokuwa wakisafiri katika behewa la treni maalum kwa ajili ya wanawake nchini India, wamejikuta wakipewa adhabu ya kupiga push up, na kinamama wenye hasira.

Treni za India huwa na behewa lisilopungua moja maalum kwa ajili ya wanawake, katika mfumo wa usafiri wa mji mkuu, Delhi.

Image caption Behewa maalum la wanawake nchini India

Hatua hiyo ilitokana na wanawake wakazi wa mji huo na hata watalii kulalamika kunyanyaswa kijinsia wanapotumia usafiri huo wa umma, kutokana na watu kujazana ndani ya mabehewa..

Gazeti la Times of India limekaririwa likisema polisi waliendesha msako katika kituo cha treni cha Gurgaon, katika viunga vya mji wa Delhi, kufuatia malalamiko kutoka kwa kinamama. Kinamama pia waliungana na polisi katika msako huo.

Walipowakamata wanaume hao ndani ya behewa walitolewa na kinamama hao wenye hasira na kuamriwa kupiga pusha up zisizo na idadi.

Image caption Push up kibao...

The Times limesema mbali na adhabu hiyo ya kijasho, wanaume hao walipigwa faini ya rupia mia mbili na hamsini, sawa na dola tano na nusu.

Kamanda wa polisi wa Gurgao S Deswal ambaye aliongoza msako huo, ameliambia gazeti la Times kuwa "Tulikuta abiria wengi wa kiume ndani ya behewa. Mara tu wanawake walipotuona, wakapata nguvu ya kuwafunza adabu wanaume hao."

"Tunataka wasichana wetu na kinamama wawe wanajiamini wanapotumia treni," amesema kamanda huyo.

Halafu unasema usafiri wa matatu au daladala mgumu...

kujiamsha kwa risasi

Bwana mmoja nchini Marekani ambaye huamka na kutembea akiwa usingizini, amejiamsha kwa mtindo wa aina yake. Bwana huyo Sandford Rothman wa Boulder huko Colorado, alisikia mlio mkubwa,wakati akiwa ndotoni, na aliposhituka akakuta amejipiga risasi kwenye goti lake.

Image caption Milimita 9

Kwa mujibu wa polisi wa huko, Bwana Rothman, mwenye umri wa miaka sitini na mitatu, huweka bastola yake ndogo yenye milimita 9, karibu na kitanda chake. Gazeti la Telegraph limesema hakuna ulevi au dawa zozote za hospitali zimehusishwa na tukio hilo.

Bwana huyo alitibiwa majeraha yake katika hospitali ya jamii ya Boulder kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Image caption 'Mguu wa kuku'

Tukio hili limekuja, siku chache baada ya bwana mwingine Darrel Elam pia wa Marekani kujipiga risasi, baada ya kuweka bastola yake kwenye mfuko wa nyuma wa suruali. Darrel alifyatua kwa bahati mbaya bastola hiyo, ambapo risasi ilipita kwenye kalio lake la kushoto, na kuteremka kupitia mguu hadi kwenye goti.

Waswahili wanasema, mtoto akililia wembe, mpe, inawezekana kabisa, jamaa hawa hawakupewa wembe walivyokuwa wadogo.

Timu mbovu zaidi duniani?

Timu moja ya soka ya kijiji hapa Uingereza, imepata umaarufu wa kuwa timu mbovu zaidi, labda hata duniani kote, baada ya kuchabangwa magoli mia mbili na ishirini na saba, katika mechi zake kumi na moja iliyocheza.

Image caption Tandaza soka

Gazeti la Metro limesema licha ya timu hiyo kufungwa mabao hamsini na tano kwa bila katika mchezo mmoja, wachezaji wa klabu hiyo ijulikanayo kama Madron FC, wana ari na moyo wa kusakata soka.

Katika mchezo huo waliobugizwa mabao hamsini na matano, wachezaji saba tu walifika uwanjani, ambapo kipa hakutokea, na hivyo kuwalazimu kucheza bila golikipa.

Image caption Nyavu zilitikisika ile mbaya

Meneja wa kikosi hicho chenye ari kubwa Alan Davenport, ambaye anashikilia wadhifa huo kwa muda amesema, inawezekana kuwa timu yake ndio mbovu zaidi Uingereza, lakini amewapongeza sana wachezaji wake kwa kujitokeza.

Aidha meneja huyo katika mahojiano na gazeti la Cornish Guardian amesema timu yake itaendelea kupambana.

"Timu hushuka daraja kila wakati, lakini sisi hatujawahi kukosa mchezo hata mmoja, tutaendelea. Huu ni wakati mgumu kwentu, lakini sio sababu ya sisi kuacha kucheza." amesema kocha Alan.

Licha ya timu hiyo kufanikiwa kupata magoli mawili katika mechi zake hizo, bado habari zake zimegonga vichwa vya habari katika kona zote za Uingereza.

Image caption Kitu!

Hata hivyo, cha kushangaza ni kuwa timu hiyo sio ya mwisho katika msimamo wa ligi ya daraja la pili ya Cornish Mining League, kwani kuna timu iitwayo Storm FC ndio inayoburuza mkia, baada ya kunyanganywa pointi kutokana na kutotokea kucheza moja ya mechi za ligi hiyo. Madron FC ina maskani yake karibu na Penzance, kusini magharibi mwa England.

Kwa hiyo usiumie sana roho kama wewe ni shabiki wa Manchester United, ambayo ilifungwa vigoli vinne juzujuzi na West Ham, au wapenzi wa Real Madrid, waliofungwa kwa taabu vigoli vitano tu na Barcelona, au Harambee stars...

Ukisikia uchungu, wewe kumbuka Madron FC, Hamsini na tano kwa bila.

Na kwa taarifa yako.....Qatar ndio taifa dogo zaidi kuwahi kupewa nafasi ya kuandaa michuano ya Kombe la Dunia.

Tukutane wiki ijayo.... Panapo majaaliwa.

Taarifa kutoka mitando mbalimbali ya habari