Tuzo ya Nobel yasusiwa

Uchina na nchi nyingine 18 zimesema hazitahudhuria sherehe ya tuzo ya Nobel itakayofanyika Ijumaa, atakayotunukiwa mkosoaji wa Uchina Liu Xiaobo, imesema kamati ya Nobel ya Norway.

Image caption Xiaobo akiwa na mkewe

Urusi, Saudi Arabia, Pakistan, Iraq na Iran ni miongoni mwa nchi zilizosusia.

Maafisa wa Uchina awali walisema "nchi nyingi" duniani zitasusia sherehe hiyo.

Sababu mbalimbali

Kamati ya Nobel inamuelezea Bw liu kama "ishara ya mbele" ya vita vya kuda haki za binaadam nchini Uchina.

Katika taarifa yake, imesema wawakilishi kutoka Urusi, Kazakhkstan, Colombia, Tunisia, Saudi Arabia, Pakistan, Serbia, Iraq, Vietnam, Afghanistan, Venezuela, Ufilipino, Misri, Sudan, Ukraine, Cuba na Morocco hazitahudhuria hafla hiyo kutokana na "sababu mbalimbali".

Kamati hiyo imesema nchi mbili zaidi, Sri Lanka na Algeria hazijatoa jibu, na kuwa nchi 44 zitahudhuria.

Afisa wa juu kabisa wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binaadam, Navi Pillay, ameshutumiwa kwa kusema hatohudhuria.

Msimamo

Kwa kulinganisha, taarifa hiyo imesema mabalozi 10 hawakuhudhuria kwenye sherehe za mwaka 2008 ambapo rais wa zamani wa Finland na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Martti Ahtisaari alitunukiwa.

Wakati huohuo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uchina Jiang yu amesema zaidi ya nchi 100 zinaunga mkono msimamo wa Beijing.

"Hao katika kamati ya Nobel wanakuza suala la kuitenga Uchina wenyewe," Bi Jiang amesema.