Muasisi wa Wikileaks akamatwa London

Muasisi wa mtandao wa Wikileaks Julian Assange amekamatwa mjini London.

Image caption Julian Assange

Polisi wamesema Bw Assange ambaye anasakwa na Sweden kuhusiana na tuhuma za ubakaji alikamatwa siku moja baada ya kutolewa kwa hati ya kumkamata.

Bwana Assange anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

Mtandao wa Wikileaks umekuwa ukichapisha taarifa za siri za mawasiliano ya ubalozi wa Marekani katika nchi mbalimbali jambo ambalo limeikasirisha na kuiaibisha Marekani.

Awali wakili wa Assange, Mark Stephens aliiambia BBC, alikuwa tayari kuzungumza na polisi wa Uingereza lakini haviamini vyombo vya sheria za Sweden.

Wakili huyo alisema hajaridhishwa na jinsi waendesha mashtaka wa Sweden wanavyochukulia kesi hiyo, kwa kuwa hawajamwambia Bw Assange ni ushahidi upi wanao dhidi yake.

Mbali na hayo wakili huyo amesema taarifa zaidi za siri zitachapishwa na Wikileaks.