Mazungumzo ya Kinuklya Iran yaendelea

Image caption Kiongozi wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo kuhusu mpango wake wa kinuklya Saeed Jalili, kushoto, awasili tayari kwa mkutano na waakilishi wa mataifa sita yenye uwezo mkubwa duniani kuanza mashauri mjini Geneva.

Waakilishi kutoka mataifa wanachama wa baraza la usalama la umoja wa mataifa watakutana kwa siku ya pili na ya mwisho kufanya mashauri ya kutatua mgogoro wa kinuklya wa Iran.

Mazungumzo ya jana jumatatu kuhusu mpango wa kinuklya wa Iran yalikuwa ya kwanza kufanyika kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Wanadiplomasia walitumia takriban saa kumi kufanya mazungumzo na mashauri.

Lakini ni bayana kwamba matatizo ya mwongo uliopita bado hayajatatuliwa na siku moja pekee ya mazungumzo mjini Geneva.

Mmoja wa maafisa katika mkutano huo alitoa kauli ya kutamausha kuhusu mkutano huo, akisema hakuna mafanikio yaliyopatikana.

Wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa pamoja na Ujerumani wanaitaka Iran kuheshimu baadhi ya maazimio ya umoja wa mataifa yanayoitaka Iran kukomesha kurutubisha madini ya Uranium.

Nchi kadhaa zinasema kuwa zinahofia hiyo huenda ni hatua ya kwanza kwa Iran kujenga zana za kinuklya. Lakini Iran inasisitiza kuwa mpango wake wa kinuklya ni wa amani.