UN: Hali nchini Ivory Coast bado ni tete

Image caption Umoja wa mataifa na umoja wa Afrika unashinikiza rais Gbagbo kuondoka madarakani.

Akizungumza kabla ya maandamano yaliyopangwa na wafuasi wa mmoja wa wagombea wawili wanaodai kushinda uchaguzi nchini Ivory Coast, katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon meonya kuwa hali huenda ikawa mbaya zaidi na kupelekea kuzuka kwa machafuko makubwa nchini humo.

Wafuasi wa bwana Alassane Ouattara wanasema baadaye leo Alhamisi watajaribu kukiteka kituo cha Televisheni ya kitaifa; na kusisitiza kuwa maandamano yao yatakuwa ni ya amani.

Jeshi ambalo linathibitiwa na mpinzani wa bwana Outtara; rais wa sasa Laurent Gbagbo limewashutumu waandamanaji hao kwa kuchochea makabiliano kimakusudi.

Ban Ki Moon ametaka pande zote mbili kujiepusha na vitendo vyovyote vitakavyoleta vurugu.

Bwana Ouattara anaaminika na wengi kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi wa urais uliofanyika nchini humo hivi maajuzi na bwana Ban amekariri wito wake wa kumtaka bwana Gbagbo ajiondoe madarakani.

Image caption Jeshi la Ivory Coast limegawanyika

Tume ya uchaguzi nchini Ivory Coast ilimtangaza bwana Ouattara kuwa ndiye mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi iliyofanyika nchini humo.

Lakini bwana Gbagbo ambaye amehudumu kama rais wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa zao la coacoa kwa kipindi cha miaka kumi amedinda kung'atuka madarakani.

Mzozo huo unatishia tena kulirejesha taifa hilo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotishia kuligawanya mara mbili.

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika unamtambua bwana Outtara ambaye amegeuza mkahawa mmoja mjini Abidjan kuwa ndiyo makao makuu ya serikali yake kama ndiye aliyechaguliwa kihalali katika uchaguzi huo.