Manchester United yailaza Arsenal 1-0

Bao la Ji-Sung Park katika kipindi cha kwanza, lilitosha kuipatia ushindi Manchester United dhidi ya Arsenal na kuwawezesha kushikilia usukani wa ligi kutoka kwa mahasimu wao hao.

Image caption Park-Ji Sung

Mshambuliaji huyo wa Korea Kusini, alifunga bao safi kwa kichwa, baada ya pasi ya Nani ambayo ilimgonga Gael Clichy na kumzidi kimo mlinda mlango wa Arsenal, Wojciech Szczesny.

Wayne Rooney angeweza kuongeza bao la pili, lakini mkwaju wake wa penalti baada ya Clichy kuunawa mpira, ukapaa juu ya lango la Arsenal.

Nafasi nzuri kwa Arsenal ilikuwa ni ya Marouane Chamakh, ambaye alikosa kufunga baada ya mpira wa kichwa alioupiga kuzuiwa na Nemanja Vidic.

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, atakuwa amesikitishwa kutokana na timu yake kushindwa kufunga kutokana na nafasi walizokuwa wakitengeneza wachezaji wake, ingwa kwa upande wa Sir Alex Ferguson atakuwa mwenye furaha kutokana na soka nzuri iliyooneshwa na wachezaji wake.

Kufungwa kwa Arsenal ina maana hadi sasa katika michezo 11 iliyopita dhidi ya Manchester United na Chelsea, haijaweza kushinda hata mmoja, hali inayotia mashaka kwa kiwango hicho kuweza kunyakua ubingwa wa England.

Kwa matokeo hayo, Manchester United sasa wamefikisha pointi 34 wakiwa na mchezo mmoja mkononi, wakifuatiwa na Arsenal yenye pointi 32, sawa na Manchester City iliyo nafasi ya tatu na Chelsea watakaopambana na Manchester United siku ya Jumapili ijayo wapo nafasi ya nne na pointi 31.