Barcelona mkataba mnono na Qatar

Barcelona imevunja mwiko katika historia yake ya miaka 111 kukataa kuvaa fulana zenye kudhaminiwa kibiashara, baada ya kuingia mkataba wa kibiashara wa paundi milioni 125 na Mfuko wa Qatar.

Image caption Lionel Messi

Klabu hiyo ilikuwa ikivaa fulana zenye nembo ya Unicef kwa miaka mitano iliyopita na shirika hilo la kuhudumia watoto sasa litashirikiana na wadhamini wapya kuweka nembo yao katika fulana za timu hiyo.

Barcelona inakabiliwa na deni kubwa, lakini kwa sasa inadai "ndio timu kubwa kuwa na udhamini katika soka duniani".

Mkataba huo mpya una thamani ya paundi milioni 25 kwa mwaka kuanzia msimu ujao hadi mwaka 2016.

Mwezi wa Julai, ukaguzi wa mahesabu uligundua deni la Barcelona ni paundi milioni 369.5 baada ya hasara ya zaidi ya paundi milioni 64.36 kwa msimu wa mwaka 2009/10.

makubaliano ya mkataba mpya yatawezesha kumpatia kocha wa Barcelona Pep Guardiola kununua wachezaji- ambaye alifanya kazi kubwa ya ubalozi kwa Qatar na kufanikiwa kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2022.

Mfuko huo wa Qatar ama Qatar Foundation, hauendeshwi kibiashara na unajihusisha na miradi ya kuendeleza elimu eneo la Mashariki ya Kati.

Mwenyekiti wake ni Sheikha Mozah Bint Nasser Al-Missned, mke wa mfalme wa Qatar.

Manchester United na Real Madrid zote kwa pamoja wanapokea paundi milioni 20 kwa mwaka kutokana na mikataba yao, huku Bayern Munich inachota paundi milioni 23.