Wafuasi wa Ouattara washambuliwa I Coast

Maafisa wa usalama nchini Ivory Coast wameshambulia wafuasi wa Allasane Ouattara anayeaminika na wengi ndiye aliyeshinda uchaguzi mkuu wa hivi karibuni.

Image caption Wafuasi wa Gbagbo na Ouattara walipokabiliana Abidjan

Shambulio hilo limetokea huku wafuasi hao wakijaribu kuteka kituo cha televisheni cha taifa.

Milio ya risasi imesikika kwenye mji mkuu Abidjan, huku milipuko ikiripotiwa karibu na hoteli moja ambako kuna afisi ya Bwana Ouattara.

Takriban watu watatu inasemekana wamekufa na wengine zaidi kujeruhiwa. Wafuasi wa Bwana Outtara walikwenda kuteka kituo hicho cha televisheni kwa sababu wanasema kinatumiwa na mpinzani wa kigogo wao Laurent Gbagbo, anayekataa kukubali alishindwa kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi uliopita.

Siku ya Jumatano Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alionya huenda kukawa na machafuko nchini Ivory Coast, iwapo hali ya vuta nikuvute inayoendelea nchini humo haitasuluhishwa kwa haraka.