Tevez asisitiza ataondoka Man City

Carlos Tevez amesisitiza ataondoka Manchester City kwa sababu uhusiano wake na "baadhi ya viongozi" ndani ya klabu, "umeharibika kiasi hakutakuwa na suluhu ".

Image caption Carlos Tevez asisitiza ataondoka

City imekataa barua ya maombi ya kutaka kuhama kutoka kwa mshambuliaji huyo raia wa Argentina, anayeelezwa anataka kuhama Man City kwa sababu za kifamilia.

Amesisitiza hana "matatizo binafsi" na meneja Roberto Mancini.

Lakini Tevez amesema: "Ni kitu nilichokuwa nikifikiria kwa muda na nimetumia muda mrefu kufikiria suala hili hadi uamuzi huu."

Katika taarifa yake, nahodha huyo wa Manchester City - ambaye alijiunga na Man City kutoka kwa mahasimu wao wakubwa Manchester United miezi 17 iliyopita, amemshukuru mmiliki wa klabu hiyo Sheikh Mansour kwa "kumuelewa na kumuunga mkono".

Tevez pia amebainisha kwamba awali aliomba kuhama klabu hiyo, msimu wa kiangazi, lakini akashawishiwa asifanye hivyo na mshauri wake wa muda mrefu Kia Joorabchian.

Man City imemnyooshea kidole mfanyabiashara raia wa Iran Joorabchian, wakielezea matendo yake kuhusiana na hali ya Tevez kwamba "inavunja moyo".

Tevez amezidi kueleza: "Nimevunjwa moyo kwamba utawala wa klabu kuelezea suala hili kwa mtazamo tofauti kabisa.

"Uhusiano wangu na baadhi ya viongozi wakuu wa klabu pamoja na baadhi ya watu ndani ya klabu, umevunjika na sasa umefikia hatua ya kutokuwepo suluhu. Nisingependa kueleza zaidi katika suala hili kwa wakati huu. Wanafahamu, kwa sababu nimewaeleza."

City wamedai wamefanya kila wawezalo kumsaidia mchezaji huyu anayelipwa mshahara mkubwa, ambaye watoto wake wawili wa kike wanaishi Argentina, wakiwa hawataki kuishi Uingereza.