Theluji yavuruga mechi za Ligi England

Mechi ya Jumamosi ya Ligi Kuu ya soka ya England, kati ya Arsenal na Stoke iliyokuwa ichezwe katika uwanja wa Emirates imefutwa kwa sababu ya "hali mbaya ya hewa."

Image caption Uwanja wa Emirates wa Arsenal

Taarifa iliyotolewa kupitia mtandao wa Arsenal, imesema uamuzi wa kufuta mechi hiyo umechukuliwa na mwamuzi wa mchezo, Lee Mason, mchana wa Jumamosi.

Theluji inayokadiriwa kufikia inchi tatu ilianguka kati ya saa tano na saa sita mchana, kukiwa hakuna dalili kama theluji hiyo nzito kama itapungua.

Uwanja wa Emirates una mfumo wa kutoa joto chini ya arhi inayofanya uwanja uweze kuchezeka, lakini hali nje ya uwanja si salama.

Nayo mechi ambayo Liverpool ingewaalika Fulham nyumbani, imeahirishwa kutokana na barafu kung'ang'ania eneo la uwanja wa Anfield.

Image caption Uwanja wa Anfield wa Liverpool

Kiasi cha theluji iliyofikia inchi 10 iliyomwagika usiku kucha, kaskazini magharibi mwa England na baridi kuwa kali sana ndio imesababishal mchezo huo kufutwa.

Mchezo huo ulifutwa baada ya maafisa wa klabu kukutana na kushauriana na polisi.

Msemaji wa klabu ya Liverpool amesema, "Ingawa uwanja unachezeka, lakini hali kuzunguka eno la uwanja si salama.

Ratiba ya mechi kati ya Birmingham na Newcastle katika uwanja wa St Andrews nayo imefutwa kutokana na wingi wa theluji na baridi kali. Taarifa ya klabu ya Birmingham imethibitisha.

Image caption Hekaheka uwanja wa St Andrews

Wafanyakazi wa uwanja wa Birmingham, wamekuwa wakifanya jitahada kubwa kuhakikisha uwanja unachezeka, lakini ilishindikana kutokana na wingi wa theluji iliyomwagika.

Mechi nyingine iliyoingia katika mkumbo wa kufutwa ni ile kati ya Wigan na Aston Villa, kutokana na sababu za usalama kutokana na theluji inayomwagika kwa wingi na baridi kali. Taarifa ya mtandao ya klabu ya Wigan imefahamisha.

Uwanja wa Wigan wa DW Stadium, unaweza kuchezeka kutokana na kuwa na mfumo wa kuupasha moto chini ya uwanja.

Lakini uamuzi ulifikiwa na polisi kutokana na sababu za kiusalama katika eneo hilo, usafiri na pia barabara zimethirika.