Nigeria yamuua 'kiongozi wa utekaji'

Mtu anayetuhumiwa kuwa kiongozi wa magenge ya utekaji nyara katika jimbo la Abia nchini Nigeria, ameuawa, kwa mujibu wa taarifa za kijeshi.

Msemaji wa jeshi Sagir Musa amesema kikosi cha kijeshi kilimpiga risasi na kumuua Obioma Nwankwo, ambaye pia anajulikana kama Osisikankwu, katika mapigano ya risasi kwenye msitu mmoja.

Nwankwo alikuwa akitafutwa kwa miezi kadhaa, baada ya kuongezeka kwa utekaji nyara na wizi katika eneo hilo.

Waandishi wa habari wanasema, watu walianza kusherekea katika mji wa Aba, baada ya kusikia taarifa za kifo chake.

Utekaji nyara umekuwa ukitokea mara nyingi katika jimbo la kusini - mashariki, kiasi kwamba familia za kipato cha kati nchini Nigeria zinalazimika kusafiri zikiwa na walinzi wenye silaha.

Mateka huachiliwa bila kudhuriwa baada ya kikombozi kulipwa.