Tanzania yashinda Cecafa

Tanzania imeshinda kombe la Cecafa baada ya kuitandika Ivory Coast kwa bao 1-0 jijini Dar es salaam, siku ya Jumapili.

Image caption Ushindi baada ya miaka 16

Ivory Coast ilikuwa ikishiriki kama timu ya kualikwa na sio mwanachama wa Cecafa.

Kilimanjaro Stars ilipata ushindi huo kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Shadrack Nsajigwa.

Ushindi huu umeipa Tanzania kombe la kwanza kabisa katika kipindi cha miaka 16.

Kocha wa Stars Jan Poulsen amefurahishwa na jinsi timu hiyo ilivyocheza vizuri jinsi michuano ilivyokuwa ikiendelea.

"Tulianza taratibu lakini tumekuwa tukicheza vizuri katika kila mchezo, na haya ndio matunda yake," amesema paulsen.

"Tumeshutumiwa siku za nyuma, lakini tumeonesha kuwa sisi tuna hadhi ya kuwa mabingwa, hatimaye."

Kocha wa Ivory Coast koaudio Georges amesema amefurahishwa na kikosi chake kichanga, ambacho bila shaka kitashiriki katika michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wasiocheza nje ya Afrika, (CHAN).

"Tulikuja hapa kujifunza, na tunarejea nyumbani tukiwa na uzoefu mkubwa," amesema.

Ivory Coast, Zambia na Malawi, walicheza kama nchi waalikwa, na kutumia michuano ya Cecafa kama sehemu ya matayarisho ya michuano ya CHAN itakayofanyika Sudan, mwakani.

wakati huohuo, Uganda ilichukua nafasi ya tatu baada ya kuifunga Ethiopia 4-3 katika mchezo uliokuwa wa kuvutia.