Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Party za Krismasi

Image caption Krismasi

Wafanyakazi wengi wanadhani sherehe za kiofisi za Krismasi zitaharibiwa iwapo wakuu wa kazi nao watahudhuria sherehe hizo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa, mbali na wafanyakazi kona kwamba hawataweza kufanya vituko vyao, pia wanakuwa na mashaka ya nguo watakazovaa, ambazo huenda mabosi wao wakawa waharidhiki nazo sana. Utafiti huo umefanywa na mgahawa wa TGIF. Katika watu elfu mbili waliohojiwa, asilimia 27 walisema wana wasiwasi huenda wakashindwa kujizuia kusema jambo ambalo halitamfurahisha mkuu wake wa kazi -- hasa baada ya kuwa wamepata kinywaji.

Wengine hata wamehisi kuwa huenda wakazusha ugomvi wa kurushiana makonde. Robo ya watu hao wamesema kuwepo kwa bosi wao kunapunguza watu kuwa na raha, wakati mmoja kati ya watu watano wamesema ni bora mabosi hao wasihudhurie kabisa sherehe hizo.

Asilimia moja ya watu hao wamesema walilazimika kuacha kazi baada ya party hizo za kiofisi za mwisho wa mwaka. Mkurugenzi wa mauzo wa TGIF Darrel wade amesema "sherehe za kiofisi za Krismasi ni watu kufurahia na kusherekea kwa kazi walizofanywa kwa mwaka mzima.-- Mabosi wanaotaka kwenda katika sherehe hizo, wanatakiwa wawaachie huru wafanyakazi wao."

Usingizi relini

Bwana mmoja nchini Japan, baada ya kutoka katika matembezi yake ya usiku ambapo alikuwa amekunywa pombe kikamilifu, alipitiwa na usingizi wakati akirejea nyumbani na kulala juu ya reli.

Image caption Reli

Bwana huyo kutoka Chiba Prefecture , mapema wiki hii aliuchapa usingizi kisawasawa katikati ya mataruma ya reli na kuanza kukoroma.

Dereva wa treni ya mizigo iliyokuwa ikipita katika reli hiyo, aliweza kumuona bwana huyo , na mara moja akaweka breki za dharura kuisimamisha treni hiyo iliyokuwa katika mwendo wa kasi.

Kwa bahati mbaya, au nzuri, treni hiyo ilishindwa kabisa kusimama, na kupita juu ya mlevi huyo, ambaye aliendelea kukoroma bila kujua kinachotokea. Baadaye mlevi huyo alishituka, na kukuta behewa la treni limesimama juu yake, na hivyo kulazimika kutambaa na kutoka chini ya treni hiyo.

Mtandao wa habari wa Japanator umesema wachunguzi wanasema, bwana huyo ana bahati kubwa kwani kulikuwa na nafasi ya kutoka kati ya trenni ya reli, la sivyo angesagwasagwa. Tukio hilo lilisababisha kuchelewa kwa treni tatu kwa karibu dakika kumi na nne, na kusababisha usumbufu kwa abiria wapatao mia saba.

Polisi sanamu

Sanamu moja lililovalishwa nguo za kipolisi na kofia yake, na kuwekwa katika kibanda cha vioo cha polisi, limezua sokomoko nchini Uchina. Kwa mujibu wa mtandao wa Guangzhou Daily, tukio hilo limetokea katika jiji la Putia, katika jimbo la Fujian mashariki mwa Uchina. Guangzhou imechapisha picha ya sanamu hilo likiwa ndani ya moja ya vibanda vinavyotumiwa na polisi kwa ajili ya kuweka ulinzi katika maeneo mbalimbali jijini humo.

Picha hiyo imeonesha polisi huyo mwanasesere akiwa peke yake ndani ya kibanda hicho. Utafiti zaidi wa vyombo vya habari nchini humo viligundua baadaye kuwa, sanamu hilo liliwekwa hapo kuchukua zamu ya ulinzi, kutokana na ukosefu wa polisi wa kutosha jijini humo.

Sanamu hilo hata hivyo liliondolewa baada ya kumaliza zamu yake ya ulinzi. Maoni mbalimbali yametoklewa kuhusiana na tukio hilo, wengine wakisema ni ubunifu wa aina yake, huku wengine wakishutumu na kusema wanawalaghai watu kuhusu usalama wao.

Mti wa Krismasi wa thamani zaidi

Image caption Mti wenye thamani zaidi

Hoteli moja mjini Abu Dhabi, katika Falme za Kiarabu imetengeneza mti wa Krismasi, wenye thamani zaidi duniani. Mti huo una thamani ya dola milioni kumi na moja.

Mti huo umepambwa na vito vya thamani ikiwa ni madini na taa za kuvutia za rangi mbalimbali. Taarifa zinasema mti wenyewe tu unathamani ya dola milioni kumi, na madini na vito vya thamani ndio vimeongeza thamani hiyo na kufikia milioni kumi na moja.

Meneja mkuu wa hoteli hiyo Hans Olbertz amesema kila mwaka huwa wanaandaa mti wa Krismasi, lakini mwaka huu wanataka kufanya kitu tofauti. Meneja huyo amesema wanawasiliana na taasisi ya Guiness ya rekodi za dunia, kuona kama mti huo utavinja rekodi ya kuwa mti wa Krismasi wenye thamani zaidi dunaini.

Mapambo katika mti huo ni pamoja na Mikufu na saa za thamani, almasi, na lulu, pamoja na mawe mengine ya thamani. Mti huo umewekwa katika baraza kubwa la hoteli ya Emirates Palace yenye vyumba mia tatu na mbili.

Alipoulizwa kuhusu ulinzi wa mti huo, Hazem Harfoush amesema mti huo ni uthibitisho kuwa Abu Dhabi ni salama. Na hoteli hiyo ni salama zaidi Bwana Harfoushameiambia BBC. "tuna walinzi hapa saa ishirini na nne, walinzi wanne, pamoja na camera za ulinzi.

Na kwa taarifa yako.....Kadi ya kwanza ya Krismasi ilitengenezwa na John Horsley mwaka 1840, na haikuuzwa hadi mwaka 1843.

Mwenzetu Dayo Yusuf anapata jiko wikendi hii, hongera sana kijana---

Nakutakia Heri ya Krismasi..

Tukutane Wiki Ijayo....Panapo Majaaliwa

Taarifa kutoka mitandao mbalimbali