Man United yazidi kung'ara kileleni

Dimitar Berbatov aliipatia Manchester United mabao mawili rahisi dhidi ya Sunderland na kuzidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England.

Image caption Dimitar Berbatov

Berbatov alipachika bao la kwanza kwa kichwa baada ya pasi ya Wayne Rooney dakika ya tano kipindi cha kwanza na baada ya hapo Manchester United wakaumiliki vyema mchezo.

Berbatov tena kipindi cha pili akapachika bao la pili baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Anderson.

Baada ya bao hilo, Sunderland waliochezesha wachezaji wengi wa akiba, hawakuonekana kufanya jitahada kubwa kutafuta mabao.

Kwa matokeo hayo Manchester United wanashikilia usukani wa msimamo wa Ligi Kuu ya England wakiwa na pointi 37.

Nao Manchester City wakicheza ugenini dhidi ya Newcastle, walifanikiwa kufunga mabao mawili dakika tano za mwanzo na kurejea katika mbio za kuwania ubingwa, baada ya wiki iliyopita kulazwa mabao 2-1 na Everton.

Bao la kwanza la Manchester City lilifungwa na Gareth Barry dakika ya pili, kabla ya Carlos Tevez kuongeza la pili dakika ya tano.

Image caption Carlos Tevez

Kipindi cha pili Newcastle walicharuka na Andy Caroll katika dakika ya 71 akaipatia New Castle bao moja.

Dakika kumi baadae Carlos Tevez akaifungia Man City bao la tatu.

Kwa matokeo hayo, Manchester City imepanda hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi 35.

Matokeo mengine Blackburn walilazwa mabao 2-0 na Stoke wakiwa nyumbani kwao. Stoke City sasa wamesogea hadi nafasi ya nane.

Image caption Wachezaji wa Stoke wakishangilia bao

Bolton wakicheza kwao wamezidi kujiimarisha katika nafasi ya tano baada ya kuwalaza West Brom mabao 2-0, na Wolves ambao sasa wanashikilia mkia wa msimamo wa ligi, walishindwa kuutumia uwanja wa nyumbani baada ya kulazwa mabao 2-1 na Wigan.

Image caption Carlton Cole

Katika mchezo wa mapema, West Ham wakicheza ugenini, walipata ushindi mnono baada ya kuwalaza Fulham mabao 3-1 na kukwamuka mkiani, ingawa bado wapo eneo la hatari la kuteremka daraja.