Basi la abiria lalipuliwa Nairobi

Mlipuko mwingine uliotokea Nairobi karibuni
Image caption Mlipuko mwingine uliotokea Nairobi karibuni ambapo polisi mmoja aliuwawa

Takriban watu sita inaarifiwa kujeruhiwa mjini Nairobi katika mlipuko ndani ya basi moja lililokuwa linajitayarisha na safari ya kuelekea mjini Kampala Uganda.

Mwandishi wa BBC David Ogot alifika kituoni hapo na anaarifu kushuhudia majeruhi kadhaa wakipelekwa hospitali;madirisha yaliyopasuliwa na mlipuko huo na damu kutiririka katika eneo hilo.

Polisi ya Kenya inathibitisha watu kujeruhiwa lakini bado haisemi chochote kuhusu milipuko hiyo ilisababishwa na nini.

Taarifa za awali za kituo kimoja cha televisheni zimeelezea mlipuko huo kusababishwa na maguruneti yaliyoachwa na mtu ambaye alitaka kupanda kwa nguvu basi hilo.

Kituo kingine cha televisheni nchini Kenya kiliripoti kwamba washambuliaji wawili waliuwawa kwa kupigwa risasi.

Polisi ya Uganda ilikwishatoa onyo hivi majuzi kwa raia wake kujihadhari na mashambulizi ya kigaidi hasa wakati huu wa kampeni za uchaguzi.