Wakimbizi wa Sudan warudi kwa wingi

Tangu mwaka 2005, shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi limesaidia katika kuwarejesha nyumbani zaidi ya watu milioni mbiliu waliopoteza makaazi yao kusini mwa Sudan. Ingawaje kasi ya operesheni hiyo ilipunguwa mwaka 2009.

Image caption Wasudan ya kusini wataka uhuru wa kujitenga

Hivi sasa ikiwa yamesalia majuma machache kabla ya kura ya maoni kuhusu Uhuru wa kujitenga kwa Sudan ya kusini, raia wengi kutoka eneo la Sudan la kusini wanaoishi kaskazini wanarudi kwao kwa wingi, takriban watu elfu 55,000 katika siku za hivi karibuni pekee.

Wengi wa wakimbizi hao, kwa mujibu wa Shirika hilo la wakimbizi, wamekuwa wakiishi katika kambi zilizouzunguuka mji wa Khartoum.

Image caption Wakimbizi wa kusini wanaoishi ndani ya kambi mjini Khartoum

Takriban wote wanaorudi hawana uhakika wa majaliwa yao kuhusu Sudan ya kaskazini wakitowa kura ya maoni kama sababu iliyowarejesha kusini. Endapo kura hiyo itapitishwa , kuna uwezekano wa eneo la kusini lenye idadi kubwa ya wakaazi Wakristu kujitenga kutoka sehemu ya kaskazini yenye Waislamu wengi.

Siku ya jumapili iliyopita Rais wa Sudan Omar al Bashir alisema kuwa serikali yake itaimarisha sheria za Kiislamu katika maeneo ya Kaskazini ikiwa kusini wataamuwa kujitenga kama Taifa huru.

Hata hivyo idadi kubwa ya watu wanaorudi kusini imewapa kibarua wahudumu wa mashirika ya misaada wanaohitaji kutoa misaada kwa watu laki mbili wasiokuwa na makaazi kufuatia mapigano yaliyotokea huko mwaka huu.

Shirika hilo la wakimbizi linapanga vituo vya mapokezi kwenye njia wanayopitia wakimbizi , ingawa limeonya kuwa wamepewa mtihani kuweza kuwatimizia mahitaji yao, kwa upande mmoja kutokana na hali mbaya ya usalama pamoja na ukosefu wa huduma za msingi.