Benki ya dunia yaibania Ivory Coast

Benki ya dunia imesimamisha msaada wa kifedha kwa Ivory Coast huku mzozo wa kisiasa ukiendelea kati ya Alassan Outtara, anayetambuliwa kimataifa kuwa alishinda uchaguzi wa urais, na kiongozi aliye madarakani Laurent Gbagbo.

Rais wa benki ya dunia Robert Zoellick amesema, mikopo kwa Ivory Coast imesimamishwa kufuatia mazungumzo baina yake na rais wa ufaransa Nicholas Sarkozy mjini Paris.

Tayari Ujerumani na Ufaransa zimewashauri raia wao walioko Ivory Coast kuondoka. Hoteli anamokaa Alassane Ouattara imezingirwa na wanajeshi waaminifu kwa Laurent Gbabgo ambaye ameendelea kukatilia madarakani licha ya Bw Gbagbo kutoa ahadi awali kwamba kutakuwa na uhuru wa kusafiri.

Hoteli hio inalindwa na wanajeshi wapatao 800 wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani, lakini wanajeshi wa Gbabgo wamefunga barabara zote zinazoelekea kwenye hoteli hiyo.

Kutokana na hali hiyo haiwezekani kupeleka bidhaa kama vile vyakula na dawa katika hoteli hiyo.

Image caption Wanajeshi wa kiskosi cha Umoja wa Mataifa

Mvutano kati ya vikosi vya umoja wa mataifa vya kulinda amani na wanajeshi waaminifu kwa Bw Gbagbo umeendelea kuongezeka baada ya Umoja wa Mataifa kuongeza mda wa vikosi vyake nchini Ivory Coast, licha ya Bw Gbabgo kuwataka waondoke mara moja.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameelezea hofu ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast, naye mkuu wa oparesheni za kulinda amani, Alan Leroy, wanaendelea kukabiliwa na hatari zaidi katika kazi zao.

Akizumgumza kwa mara ya kwanza kwenye televisheni, Bw Gbabgo ametoa wito tume ya kimataifa iundwe ili kuchunguza mzozo huo wa baada ya uchaguzi, lakini wafuasi wa Bw Outtara wamekatalia mbali pendekezo hilo, wakisema jamii ya kimataifa imeshatangaza msimamo wake kuhusu swala hilo.