Wabunge Kenya waipinga ICC

Wabunge wa Kenya wamepiga kura kutaka nchi hiyo kujitoa katika makubaliano yaliyofikiwa kuunda Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ya The Hague (ICC).

Image caption Ghasia baada ya uchaguzi 2008

Hatua hiyo inakuja wiki moja tu baada ya mwendesha mashitaka wa ICC kutaja majina sita ya watu anaowatuhumu kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi.

Orodha ya majina hayo imejumuisha wanasiasa wa ngazi za juu na wafanyakazi wa serikali.

Image caption Mwendesha mashitaka wa ICC Moreno Ocampo

Wabunge hao hawana uwezo wa kuleta mabadiliko yoyote ya haraka katika nchi kujiondoa katika makubaliano ya ICC, lakini wamefikisha ujumbe kwa serikali kuanza mchakato wa kujiondoa.

Takriban watu 1,200 walikufa na zaidi ya watu laki tano kukimbia makazi yao katika ghasia hizo zilizotokana na uchaguzi uliofanyika Disemba mwaka 2007.

Ghasia hizo zilimalizika baada ya Rais Mwai Kibaki na mpinzani wake Raila Odinga kukubali kugawana madaraka, Bw Odinga akipata wadhiwa wa waziri Mkuu.

Image caption Mwai Kibaki na Raila Odinga

Katika makubaliano ya amani yaliyofikiwa, ilikubaliwa kuwa waliosababisha ghasia hizo watafikishwa mahakamani nchini Kenya, au katika Mahakama ya Kimataifa mjini Hague.

Mwandishi wa BBC mjini Nairobi anasema iwapo serikali itaungana na wabunge, itachukua muda usiopungua mwaka mmoja kwa Kenya kujiondoa rasmi kutoka ICC, lakini kesi ambazo tayari zimefunguliwa hazitasitishwa.

Kutajwa kwa majina sita ya washukiwa kulisababisha mtikisiko mkubwa katika siasa za Kenya, anasema mwandishi wa BBC.

Image caption Wabunge wa Kenya

Katika orodha hiyo, yupo Uhuru Kenyatta, ambaye ni naibu waziri mkuu na mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya, jomo Kenyatta.

Pia wapo wanasiasa wengine wa ngazi za juu ambao ni washirika wa rais wa waziri mkuu, na pia mkuu wa zamani wa polisi.

Mtazamo wa kikoloni

katika majadiliano yaliyodumu hadi usiku, wabunge hao walisema ICC ina mtazamo wa kikoloni, ni mahakama inayopinga uafrika na kusema Kenya inauza uhuru wake.

"Ni Waafrika peke yake ndio wanashitakiwa na ICC," gazeti la kila siku la Nation limekaririwa likimkariri waziri wa nishati Kiraitu Murungi.

"Hakuma Mmarekani au Mwingereza atashitakiwa katika mahakama ya ICC, tusiruhusu kurejea wenyewe katika ukoloni," amesema.

Mbunge mmoja pekee, Martha Karua, waziri wa zamani wa sheria ndiye alikuwa na mtazamo tofauti.

"ICC haikutufuata sisi, sisi ndio tuliikaribisha," alisema Karua.

"Iwapo Wakenya wanajiuliza kuhusu kutoshitakiwa, hii ndio sura yake halisi."

Mara ya kwanza

Mwandishi wetu anasema baadhi ya wabunge wanaamini itachukua miaka mingi kwa mchakato wa kisheria katika mahakama ya ICC kuanza kufanya kazi.

Hii ndio sababu waliamua kwenda katika mahakama ya kimataifa, badala ya mahakama ya Kenya.

Mwandishi huyo anasema walishitushwa wakati mwendesha mashitaka wa ICC Louis Moreno Ocampo alipotaja majina ya washukiwa, kwa sababu kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, ilianza kuonekana kuwa wanasiasa wakubwa wasioweza 'kuguswa' huenda wakashitakiwa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii