Ecowas yaitisha Ivory Coast kijeshi

Umoja wa Kiuchumi wa nchi za Afrika Magharibi Ecowas, umemuambia rais anayetetea kiti chake nchini Ivory Coast Laurent Gbagbo kuachia madaraka, au atarajie kukabiliwa kutolewa kwa "nguvu kisheria".

Image caption Jeshi la UN likifanya doria mjini Abidjan

Taarifa hiyo imekuja mwishoni mwa mazungumzo ya dharura juu ya mzozo wa kisiasa uliozuka kufuatia kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi.

Umoja huo wenye nchi 15 wanachama, pamoja na mashirika mengine ya kimataifa yamemtambua mpinzani wa Bw Gbagbo, Alassane Ouattara kuwa mshindi wa urais.

Baraza la Katiba la Ivory Coast linasema Bw Gbagbo alichaguliwa, likisema kulikuwa na wizi wa kura katika ameneo kadhaa.

Image caption Laurent Gbagbo na Alassane Ouattara

Uchaguzi huo ulikuwa na lengo la kuiunganisha nchi hiyo, baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2002, kuligawanya taifa hilo ambalo linazalisha kakao kwa wingi zaidi duniani.

Siku ya Alhamisi, matangazo ya kituo cha televisheni cha taifa,yaliacha kuonekana katika maeneo kadhaa nje ya Abidjan.

Lakini licha ya shinikizo hilo la kimataifa, Bw Gbagbo ameendelea kun'gan'gania madarakani, akisema uamuzi wa Benki kuu ya Afrika Magharibi kutoa akaunti ya beni ya nchi kwa Bw Ouattara ni kinyume cha sheria.

Msemaji wa Bw Gbagbo, Ahoua Don Mello akisoma taarifa kupitia televisheni amesema ilikuwa ni "kinyume cha sheria na nje ya kanuni za benki, na kutakuwa na madhara makubwa".