Ancelotti awataka Chelsea sasa waamke

Meneja wa Chelsea, Carlo Ancelotti, amewaambia wachezaji wake, hawana budi "kuamka" kabla matumaini yao ya kuutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya England hayajayeyuka.

Image caption Carlo Ancelotti

Chelsea walikubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Arsenal na sasa wamecheza michezo sita ya ligi bila ushindi na wameporomoka hadi nafasi ya nne ya msimamo wa ligi.

Meneja huyo Mtaliano amesema: "Kuna machungu mengi kwa sababu kipindi kigumu bado kinaendelea kutung'ang'ania."

"Tunapoteza nafasi yetu katika msimamo wa ligi. Hatuna budi kuamka haraka iwezekanavyo."

Meneja huyo alizidi kueleza: "Nadhani tuna uwezo wa kurejea na kuutetea ubingwa wetu, lakini kamwe hayo hayawezekani kwa namna tunavyoceza sasa."

"Hatutakiwi kuwaza juu ya ubingwa, tunachotakiwa ni kufikiria namna ya kujikwamua na hali hii. Tunahitajika kujiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Bolton na tujaribu kushinda."

Ushindi wa mwisho kwa Chelsea msimu huu wa ligi, ilikuwa tarehe 10 mwezi wa Novemba dhidi ya Fulham lakini Ancelotti, aliyeiongoza klabu hiyo kushinda ubingwa wa Ligi Kuu ya England na Kombe la FA msimu uliopita, amepuuza kauli kwamba ajira yake imo mashakani.

Alipoulizwa ni kwa muda gani mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, ataendelea kuwa mvumilivu, Ancelotti alijibu: "Sijui. Kwa vyovyote vile hatakuwa mwenye furaha wakati huu."