Marais wa ECOWAS waelekea Ivory Coast

Marais watatu kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wanaanza ziara yao nchini Ivory Coast katika kile kimetajwa hatua ya mwisho kumshawishi Rais Laurent Gbagbo, kuondoka madarakani kwa njia ya amani ama sivyo aondolewe kijeshi.

Image caption Viongozi wa ECOWAS

Marais wa Sierra Leone, Cape Verde na Benin watakuwa wakiwasilisha ujumbe kutoka ECOWAS kwa Bw Gbagbo, unaomtaka akubali ushindi wa Alassane Ouattara na kumkabithi madaraka.

Wakati huo huo Muungano wa Afrika AU-umemteuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, kuwa mjumbe maalum wa muungano huo katika harakati za upatanishi wa mzozo wa Ivory Coast.

Taifa la Ivory Coast limekuwa likikumbwa na mgogoro wa kisiasa kati ya Rais Laurent Gbagbo na mtu anayetambuliwa kimataifa kushinda kita cha Urais katika uchaguzi wa mwezi uliopita, Alassane Ouattara.

Mjini Paris Ufaransa wafuasi wa Bw Ouattara walivamia ubalozi wa Ivory Coast nchini humo na kulalamikia hatua ya Bw Gbagbo kugoma kuondoka madarakani.