Kocha wa Spurs atabiri msimu mzuri

Meneja wa Tottenham Harry Redknapp amesisitiza timu yake inaweza kuwa na msimu mzuri baada ya kuwalaza Aston Villa 2-1, licha ya mshambuliaji wao wa kutumainiwa Jermain Defoe, kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Image caption Harry Redknapp

Redknapp awali aliwahi kusema timu yake inapaswa kuzingatiwa miongoni mwa timu zitakazofanya vizuri baada ya kuwa miongoni mwa timu 16 zinazowania ubingwa wa Ulaya.

Baada ya kurejea kwa mshambuliaji Rafael van der Vaart aliyepachika mabao mawili, Redknapp amesema: "Zilikuwa ni pointi tatu muhimu."

"Tulijitahadi kupigana hadi mwisho. Mchezo kama huu tuliocheza hakuna shaka yoyote, msimu huu utakuwa mzuri kwetu."

Spurs, waliocheza wakiwa 10 kwa karibu saa nzima, waliweza kuhimili vishindo vya Villa katika dakika za mwisho baada ya Marc Albrighton kufunga bao moja.

"Kumpoteza Jermain ilituweka katika wakati mgumu, lakini tulijitahidi kudhibiti mpira,"alisisitiza Redknapp.

Pointi tatu zimeihakikishia klabu hiyo ya kaskazini mwa London, kuendelea kuweka chagizo ya kuwemo miongoni mwa timu nne zitakazomaliza nafasi za juu katika msimamo wa ligi kuu ya England, wakiendelea kushikilia nafasi yao ya tano.