Marekani yaahidi kujenga Sudan Kusini

Image caption Mwanamke huyu raia wa Sudan Kusini akipiga kura ya maoni.

Rais wa marekani Barrack Obama amesifu mafanikio yaliyopatikana katika siku ya kwanza ya upigaji kura ya maoni kuhusu uhuru wa Sudan Kusini.

Amesema ilikuwa ni hatua ya kihistoria katika utekelezaji wa mkataba wa amani uliomaliza vita kati ya kaskazini na kusini mwaka 2005 -- na kwamba marekani imejitolea vilivyo kulisadia taifa jipya la Afrika linalotarajiwa kuidhinishwa na kura hiyo.

Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya marekani imetoa taarifa inayomsifu rais wa Sudan Omar al-Bashir kutokana na ahadi yake ya kukubali matokeo ya kura hiyo ya maoni. Idadi kubwa ya wapiga kura walijitokeza katika vituo mbali mbali vya kupigia kura Sudan Kusini.

Image caption Raia wengi wa Sudan Kusini wamejitokeza kupiga kura.

Raia wa Sudan Kusini wanaoishi Kaskazini pia walipiga ingawa hali haikuwa ya kuchangmka kama ilivyokuwa katika eneo la Kusini.

Upigaji kura utaendelea kwa kipindi cha siku sita zijazo.

Msemaji wa tume andalizi ya kura hiyo ya maoni, Chan Reec, amesema kumekuwa na machafuko kati ya waasi na wanajeshi wa Sudan katika jimbo la Unity lenye utajiri mkubwa wa mafuta katika eneo la mpakani kati ya Sudan Kaskazini na Kusini.