Waliosimamishwa na Fifa kukata rufaa

Wajumbe wawili wa kamati ya utendaji ya Fifa, Amos Adamu na Reynald Temarii, wamewasilisha rasmi rufaa dhidi ya adhabu ya kusimamishwa kutokana na tuhuma za rushwa.

Image caption Adamu na Temarii

Adamu ambaye ni raia wa Nigeria, amesimamishwa kwa kipindi cha miaka mitatu, baada ya kuonekana akiomba rushwa kutoka kwa waandishi waliokuwa wakimrekodi bila yeye kufahamu.

Temarii, kutoka Tahiti, alionekana hana hatia ya rushwa, lakini alifungiwa mwaka mmoja, kwa kupuuza taratibu za usiri.

Wote walikana kufanya jambo lolote baya na Shirikisho hilo la soka duniani, likasema tarehe ya kusikiliza shauri lao itathibitishwa baadae.

Wajumbe hao wawili mwezi wa Desemba walikosa kupiga kura ya kuchagua nchi zitakazoandaa fainali za Kombe la dunia mwaka 2018 na 2022.

Kamati huru ya Fifa ya kusikiliza rufaa, inayoongozwa na Rais wa Shirikisho la soka la Bermuda, Larry Mussenden, ndiyo itasikiliza rufaa hizo.

Temarii alidai siku ya Alhamisi alipokea barua kutoka Fifa tarehe 30 mwezi wa Desemba ambayo "imemfutia tuhuma zake za rushwa".

Ameongeza: "Kamati ya maadili imenituhumu kwa kukiuka maadili ya Fifa ya usiri na kuaminika, tuhuma ambazo nazikana kabisa."

Adamu ana matumaini kuitwa na kamati hiyo katika kipindi cha wiki moja, na kumsafisha kutokana na tuhuma anazokabiliana nazo, ili aweze kusimama tena katika uchaguzi ujao.

Shirikisho la soka barani Afrika (Caf) litakutana tarehe 23 mwezi wa Februari, Khartoum Sudan, ambapo watachagua wajumbe wawili kati ya wanne, watakaoingia katika kamati ya utendaji ya Fifa.

Jina la Adamu ni miongoni mwa yaliyopendekezwa, kutegemea rufaa yake.