Wenger awaita wachezaji wake "wajinga"

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ameibandika jina la "ujinga" timu yake, baada ya kufungwa bao 1-0 na Ipswich Town, katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya kuwania Kombe la Carling kwenye uwanja wa Portman Road.

Image caption Arsene Wenger

Bao la mshambuliaji wa Ipswich, Tamas Priskin, limeihakikishia timu hiyo mwanzo mzuri wakati wakijiandaa kwa mchezo wa marudio tarehe 25 mwezi huu, katika uwanja wa Emirates.

"Tulikuwa wajinga sana. Niliwaambia wachezaji kama hamtaweza kushinda mchezo huu, basi jitahidini msifungwe," alisema Wenger.

"Nimehuzunishwa sana. Hatukuwa na mchemko, hakukuwa na ubunifu. Lakini nina matumaini makubwa tutashinda katika mchezo ujao nyumbani."

Wenger anakabiliwa na tatizo la kuwakosa walinzi wa kati Thomas Vermaelen na Sebastien Squillaci, ambao wote ni majeruhi.

Lakini licha ya walinzi wakati Laurent Koscielny na Johan Djourou, kushindwa kuuzuia mpira wa juu uliopigwa na Colin Healy na kumkuta Priskin, aliyepachika bao la ushindi.

Wenger amesisitiza matokeo hayo hayatamlazimisha kununua mlinzi mwengine wa kati wakati huu dirisha dogo la usajili.

"Itakuwa hakuna la kujitetea, hatukushinda kwa sababu eti tunahitaji mlinzi wa kati, tumepoteza mchezo kwa sababu hatukucheza katika kiwango chetu cha kawaida," aliongeza Wenger.

Mlinzi wa kati wa West Ham United, Matthew Upson, ambaye alianza kucheza soka akiwa na Arsenal, amekuwa akitajwatajwa huenda akarejea katika klabu yake hiyo za ya zamani.

Wenger anaamini ratiba ngumu ambayo wamekabiliana nayo kwa muda huu, ndio sababu kubwa ya kupoteza mchezo dhidi ya Ipswin.