Beckham huenda akajiunga Spurs

Meneja wa Tottenham, Harry Redknapp atajaribu kumchukua nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya England, David Beckham kwa mkopo mwezi wa Januari kutoka klabu ya LA Galaxy ya Marekani.

Image caption David Beckham

Msimu wa Ligi ya Marekani unaanza upya tarehe 15 mwezi Machi, hali inayompa matumaini Redknapp kumsajili kwa muda Beckham mwenye umri wa miaka 35.

Redknapp amesema:"Tutawasiliana na LA Galaxy kuona uwezekano wa klabu hiyo kumuachia na iwapo David atapatikana kwa mkataba wa miezi mitatu, litakuwa jambo zuri."

Beckham mwaka 2009 na mwaka jana wa 2010, alichukuliwa kwa mkopo na klabu ya Italia, AC Milan.

Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, alizaliwa na kukulia maeneo ya kaskazini mwa London na alifanya mazoezi katika klabu ya Tottenham kabla ya kusaini mkataba wa soka ya kulipwa katika klabu ya Manchester United.