Dalglish hajapanga kusajili wachezaji

Meneja wa Liverpool Kenny Dalglish bado hajazungumza na wamiliki wa klabu juu ya usajili wa wachezaji wapya wakati huu wa msimu wa dirisha dogo la usajili mwezi wa Januari.

Image caption Kenny Dalglish

Liverpool ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, walitoka sare ya mabao 2-2 na watani wao wa jadi Everton siku ya Jumapili.

Lakini zikiwa zimesalia wiki mbili kabla ya dirisha dogo la usajili halijafungwa, Dalglish amesema: "Hakuna kilichojadiliwa kuhusiana na wachezaji wapya au jambo jingine.

Dalglish ambaye tangu achukue hatamu za uongozi wa klabu ya Liverpool, hajashinda mchezo hata mmoja- alianza kuchambua kikosi chake alichorithi kutoka kwa mtangulizi wake, Roy Hodgson, na anahisi baadhi ya wachezaji wanapaswa kupewa nafasi ya pili kuonesha uwezo wao.

Hodgson alishindwa kuifikisha Liverpool panapotakiwa na aliwasajili Paul Konchesky na Christian Poulsen, ambao wameshindwa kujiimarisha na kuonekana ni wa kutumainiwa katika kikosi cha kwanza.