Waziri wa Viwanda Kenya ajiuzulu

Waziri wa Ustawishaji wa Viwanda nchini Kenya, Henry Kosgey, ambaye alikuwa amepangiwa kufikishwa maakamani na maafisa wa taasisi ya kupambana na rushwa, amejiuzulu wadhifa wake.

Image caption Nairobi

Kosgey amechukuwa hatua hiyo siku moja baada ya Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Kenya, Amos Wako kutoa idhini kwa tume ya kupambana na ufisadi nchini humo, kumkamata na kumfungulia mashtaka kutokana na kashfa ya kuruhusu uagizaji wa magari yaliyopita muda wa kutumika nchini humo.

Bwana Kosgey ni mwenyekiti wa chama cha ODM cha Waziri Mkuu Raila Odinga na pia ni mmoja wa Wakenya sita wanaoshutumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu, ICC, kupanga machafuko baada ya uchaguzi miaka mitatu iliyopita.

Chama cha ODM hata hivyo kimesema kitaendelea kumuunga mkono Kosgey.