Dalglish huenda akadumu meneja Liverpool

Meneja mpya wa muda wa Liverpool Kenny Dalglish, atakuwa mtu ambaye huenda akapewa mkataba wa kudumu katika klabu hiyo.

Image caption Kenny Dalglish

Dalglish kwa sasa anashikilia hatamu katika klabu hiyo kwa muda hadi utakapomalizika msimu huu, huku mkurugenzi wa soka, Damien Comolli akiwa na kazi ya kumtafuta mtu atakayechukua nafasi ya Roy Hodgson, kwa mkataba wa muda mrefu.

Alipoulizwa iwapo mchezaji huyo wa zamani wa Liverpool na sasa meneja wa muda, Dalglish, atafikiriwa kwa kazi hiyo, Comolli alisema: "Jibu ni ndiyo."

Dalglish aliongeza kusema: "Iwapo nitafanya kazi yangu vizuri inavyopaswa na kama atatokea mtu mwengine atakayefanya vizuri zaidi yangu, sitakuwa na tatizo lolote."

Dalglish, ambaye enzi zake za kusakata kandanda na baadae katika nafasi ya umeneja, alishinda mataji ya ligi mara nane akiwa na Liverpool kati ya mwaka 1977 na 1991, aliomba kazi ya umeneja msimu huu ulipoanza baada ya kuondoka Rafael Benitez, lakini nafasi hiyo ikaenda kwa Hodgson.

Lakini baada ya mambo kwenda mrama kwa matokeo ya kukinaisha, mkataba wa Hodgson ukasitishwa na siku ya Jumamosi klabu ikamgeukia meneja wake huyo wa zamani, kushikilia hatamu za kuiongoza klabu hadi mwisho wa msimu.

Hali hiyo inaweza kumpatia nafasi Dalglish ya mkataba wa kudumu, wakati huu Comolli akiwa anamtafuta mtu atakayeivusha Liverpool vyema hadi mwisho wa msimu huu.