Upigaji kura waenda vizuri Sudan Kusini

Jumuia ya kimataifa imeelezea kuridhishwa na kura ya maoni inayohusu uhuru wa Sudan Kusini katika siku ya pili ya upigaji kura.

Image caption Upigaji kura ukiendelea Sudan Kusini

Kura hiyo inafanyika baada ya kutiwa saini mkataba wa amani uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe, kati ya eneo la Waarabu la Kaskazini na eneo la Kusini ambako wengi ni Wakristo.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan, ni mmoja wa waangalizi kimataifa katika kura hiyo mjini Juba. Aliambia BBC ameridhishwa na namna kura hiyo ilivyoendeshwa.

Watu katika siku ya pili hawakujitokeza kwa wingi, kama ilivyokuwa siku ya kwanza, lakini waandishi wa habari walio eneo la upigaji kura, wamesema wapiga kura bado wanaonekana na nia ya kutekeleza haki yao hiyo.

Katika siku tatu zilizopita kwenye eneo la Abyei lenye utajiri wa mafuta na linalogombewa kati ya kusini na kaskazini, kumeripotiwa watu thelathini wameuawa kufuatia mapigano yaliyozuka.

Abyei nao wanatazamiwa kupiga kura ya maoni kuamua mustakabali wao.

Kura ya maoni kuamua mustakabali wa Sudan Kusini, itaendelea kwa muda wa siku saba, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mapatano ya amani yaliyomaliza vita baina ya kaskazini na kusini mwaka 2005.