Sulley Muntari kachoshwa na Inter Milan

Mchezaji wa kiungo wa timu ya taifa ya Ghana, Sulley Muntari, anajiandaa kuihama klabu ya Italia ya Inter Milan.

Image caption Sulley Muntari

Mkurugenzi wa ufundi wa klabu ya Italia, Marco Branca, ameeleza kupitia televisheni ya nchi hiyo, kwamba Muntari mwenye umri wa miaka 26, amekwishawasilisha maombi ya uhamisho.

Enzi za Jose Mourinho, Muntari alikuwa anakaribia kupewa nafasi ya moja kwa moja ya chaguo la kwanza, katika msimu wake wa kwanza na Inter.

Hata hivyo, Muntari alipoteza nafasi yake katika timu hiyo msimu uliopita na msimu huu amecheza mara chache.

Mchezaji huyo wa zamani wa Portsmouth, amecheza mara 12 katika mashindano yote na zaidi akiwa mchezaji wa akiba.